Jumatano , 22nd Jun , 2016

Rekodi mpya ya mabao imewekwa na Lionel Messi kwa kuwa mfungaji mpya wa mara zote wa Argentina, akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Gabriel Batistuta.

Lionel Messi amekuwa mfungaji wa mara zote wa Taifa la Argentina, baada ya kuiongoza nchi yake kuifunga Marekani mabao 4-0 na kuingia hatua ya fainali ya michuano ya Copa America.

Messi alifunga bao lake la 55, kwenye mchezo huo wa Alfajiri ya leo kwenye uwanja wa NRG , na kuipiku rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mfungaji wa zamani Gabriel Batistuta mwenye mabao 54.

Mchezaji huyo mara tano wa dunia, hadi sasa amefunga mabao 5, kwenye michuano hiyo ya Copa America, na ana nia ya kuisaidia Argentina kutwaa taji hilo, walilolikosa kwa miaka 23 hadi sasa.

Argentina huenda ikakutana na Chile au Colombia kwenye fainali hiyo itakayopigwa jumapili hii kwenye uwanja wa East Rutherford, New Jersey.