Jumatatu , 20th Jun , 2016

Tetesi za Ulaya zinadai kuwa Arsenal ipo mbioni kutuma ofa kwa klabu ya Inter Milan ili iweze kuinasa saiani ya beki wake wa kati Jeison Murillo.

Beki wa Inter Milan Jeison Murillo (pichani) anayetajwa kuwaniwa na klabu ya Arsenal.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia ameng'ara akiwa na klabu hiyo ya Italia msimu uliopita akicheza mechi 35 katika michuano yote.

Lakini kutokana na matatizo ya kiuchumi ya Inter Milan, wachezaji kadhaa muhimu wanaweza kuuzwa katika msimu wa majira ya joto.

Habari hizo zimeongeza kuwa Washika Mtutu wa London wanakabiliwa na ushindani kutoka Bayern Munich na Zenit St Petersburg katika kinyang'anyiro cha kuinasa saini ya beki huyo.

Hata hivyo beki huyo kisiki alisisitiza kuwa hatajadili chochote kuhusu mustakabali wake hadi baada ya kumalizika kwa michuano ya Copa America nchini Marekani.

Arsenal inahaha katika kuhakikisha inajenga kikosi imara kitakacholeta ushindani mkubwa msimu ujao huku ikiwa imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji Granit Xhaka aliyejiunga na klabu hiyo akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani.

The Gunners pia walikua wakiwania saini ya mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy lakini kocha wa klabu hiyo Mfaransa Arsene Wenger ametamka kuwa nyota huyo atasalia na klabu yake ya sasa.