Jumamosi , 28th Mei , 2016

Kocha wa Yanga Hans van Der Pluijm, amesema anaamini Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika utabaki Tanzania kwani hawezi kufungwa kwenye mechi zote za ugenini katika michezo yote katika hatua ya makundi.

Pluijm amesema yeye pamoja na benchi zima la ufundi la klabu hiyo wameshapanga mikakati ya jinsi ya kulichukua taji hilo baada ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa kuwatoa Sagrada Esperanca ya Angola.

Pluijm amesema ushindi wa ugenini utaiweka timu pinzani katika presha ya mchezo wa kujihami katika mchezo wa nyumbani hivyo kikosi chake kitacheza kwa kutumia mapungufu ya wapinzani na kuweza kujiweka katika nafasi nzuri.

Pluijm amesema timu yake ina rekodi mbaya ya kufungwa mechi za ugenini na hilo ameliona kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo hataki kuliona likijitokeza kwenye Kombe la Shirikisho.

Pluijm amesema atahakikisha anapambama kwenye mechi zote watakazozicheza ugenini kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho ili kuhakikisha wanashinda ili kuwapa mazingira magumu wapinzani wao kwenye michezo ya nyumbani.

Pluijm amesema anaendelea kukiboresha kikosi chake ili kuhakikisha wanachukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho huku lengo hasa likiwa ni kuzima utawala wa TP Mazembe.

Yanga ipo kwenye Kundi A na timu za MO Bejaia ya Algeria, Medeama (Ghana) na TP Mazembe ya DR Congo. Kundi B zipo Kawkab na FUS Rabat zote za Morocco, Etoile du Sahel (Tunisia) na Ahly Tripoli ya Libya.

Katika rekodi zake, TP Mazembe imetwaa mara tano ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika miaka ya 1967, 1968, 2009, 2010 na 2015, pia imetwaa mara moja Kombe la Washindi ambalo kwa sasa ni Kombe la Shirikisho mwaka 1980 huku Yanga ikiwa haijawahi kutwaa ubingwa wowote wa Afrika.

Yanga itaanza mechi zake za makundi ya Kombe la Shirikisho kati ya Juni 17 hadi 19, mwaka huu kwa kucheza na Mo Bejaia ya Algeria ugenini halafu itaikaribisha TP Mazembe nyumbani kati ya Juni 28 na 29.