Alhamisi , 12th Mei , 2016

Wanamtandao wa Wanawake na Katiba/Uchaguzi na Uongozi wamelaani vikali na kusema kuwa wamesikitishwa na kufadhaishwa na hali ya udhalilishwaji na matumizi ya lugha chafu na za kejeli dhidi ya Wanawake Bungeni.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia, TGNP, Lilian Liundi,

Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia, TGNP, Lilian Liundi, imesema kuwa kauli kama hizo zinaendeleza dhuluma, udhalilishaji ana kuwanyima wanawake haki yao ya Kikatiba na kuwakosea heshima.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kilichotokea Bungeni hivi karibuni kimekuwa ni muendelezo wa matukio ya utumiaji wa lugha ya kudhalilisha wanawake bungeni na wanawake wote nchini ni kitendo ambacho hakitavumiliwa na kufumbiwa macho, na hasa wanawake, ambao wana nia ya dhati ya kujenga uwiano wa kijinsia katika ngazi za uongozi nchini.

Bi. Liundi amesema kuwa tukio hili ni kinyume na Tamko la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR:1948) Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979, na mikataba mingine ya Haki za Binadamu na Usawa wa Kijinsia ambayo nchi imeridhia.

Aidha, ameongeza kuwa suala hilo ni kinyume pia na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya 9(f),(g) na (h) na Ibara ya 12 (2) pia ni uvunjwaji wa sheria namba 15 ya mwaka 1984 ib. 6.

“Ni katika muktadha huu, tunakemea na kulaani vikali mwenendo huu ambao unarudisha nyuma harakati za kutetea haki za wanawake katika uongozi na kukiuka misingi ya utawala bora nchini.”

Ikumbukwe kuwa Bunge ni nguzo na muhimili mmojawapo mkuu katika nchi hii. Hivyo basi Bunge halipaswi kuruhusu mbunge yeyote yule (awe wa kiume au wa kike) kutumia chombo hiki muhimu kukandamiza sauti za wanawake bungeni na kuwaondoleaa hadhi ya utu wao ili wasijiamini katika uongozi na hivyo washindwe kutetea maslahi ya watanzania.

Aidha, wanamtandao huo wamesema wanatakaa kuona hatua stahiki za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya wale wote wenye tabia kama za udhalilishaji bungeni ili kukomesha mwenendo huu.

Wametoa wito kwa jamii kwa ujumla kukemea na kuwawajibisha wabunge wao ambao wamewapa kura ili wakatetee maslahi ya kimaendeleo kwa wananchi wote (Wanawake na Wanaume).