Msemaji wa Chama cha Mapinduzi, (CCM), Christopher Ole Sendeka
Ole Sendeka ameyasema hayo wilayani Longido katika mkutano wa hadhara na wananchi ambapo amesema kuwa watumishi hewa wameigharimu serikali mamilioni ya fedha hivyo watanzania na viongozi wanapaswa kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika utumbuaji wa majipu ambayo yanazorotesha maendeleo ya nchi.
Aidha, amewataka wanachama na viongozi wa CCM kuwa vinara wa kuibua ufisadi unaofanyika kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa ili Watanzania waweze kufaidi matunda ya utawala bora unaotokana na chama hicho.
Kwa upande wao Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kilumbe Ng`enda na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Lekule Laizer wamesema kuwa kwa muda wa miezi michache ya utawala wa Rais Dk. Magufuli amefanya kazi kubwa ambayo ingeweza kugharimu miaka hivyo chama hakitawavumilia wanaokisaliti chama hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Esupat Ngulupa, amesema kuwa Watanzania wana imani kubwa na Rais Dk. Magufuli na wangependa kuona kasi iyo ya utendaji ikiendelea ili kulitoa taifa kwenye utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi.
Msemaji wa Chama cha Mapinduzi amehutubia mkutano wa hadhara pamoja na kuwasimika Makamanda wa Chama hicho wilaya ya Longido ikiwa ni moja kati ya hatua za kuchochea uhai wa chama.