Jumamosi , 7th Nov , 2015

Rais Magufuli leo amekutana na baadhi ya watendaji wakuu wa serikali na kutoa uelekeo wa serikali anayoitaka mara baada ya kuapishwa ikiwa ni pamoja na kufuta safari za nje ya nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo asubuhi katika Ikulu ya Dar es Salaam amefanya kikao na Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutoa uelekeo wa serikali anayoitaka mara baada ya kuapishwa.

“Nataka Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana ya ‘HAPA KAZI TU’ na viongozi kuzingatia na kukumbuka ahadi nilizotoa ili zianze kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja” Rais Magufuli amesema.

Katika Kikao chake, Rais ametoa mwongozo na kusisitizia kuwa ni lazima kila mtendaji serikalini kuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge mbele kwa ufanisi zaidi.

Katika kikao hicho Rais ameelekeza mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili atakapo teua Baraza lake la Mawaziri mambo hayo yawe tayari ili Mawaziri watakaoteuliwa waweze kuyasimamia bila kukosa.

Mambo hayo muhimu ni kama ifuatavyo:
Kuanzia mwezi Januari mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure bila kulipa ada, Katika jambo hili, Rais amewataka watendaji kuanza kuliwekea mikakati tayari kwa utekelezaji suala la mikopo ya wanafunzi nalo lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi

Amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo atakapolitolea suala hilo maamuzi mengine na kueleza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje.

Pengine patokee jambo la dharura sana na hata hilo lazima kibali kitolewe na Rais au Katibu Mkuu Kiongozi. Badala yake Rais amewataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi wa Tanzania.

Katika Kikao hicho, Rais amemtaka Kamishna wa TRA, Ndugu Rished Bade kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kero ndogo ndogo kwa wananchi lianze kutekelezwa kama alivyo ahidi kwa kufanyiwa kazi mapema zaidi.

Rais ameitaka TRA kukusanya mapato hayo kutoka kwa wafanya biashara wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote hapa Tanzania na kusisitiza kuwa katika Serikali hii wa kutoa maamuzi vinginevyo zaidi ya haya ni yeye Rais ama Makamu wake.

Rais Magufuli pia ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa kuibia Serikali kwa watu kuongeza bei ya vitu hata kama ni vya bei ndogo kabisa katika jamii.

“Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja”. Rais amesema, na kuwataka watendaji hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia maadili mema ya kazi.

Tags: