Ijumaa , 16th Oct , 2015

Watu wawili wamefariki dunia mkoani Mbeya katika matukio mawili tofauti likiwemo la mtoto kumuua baba yake kwa kumpiga kwa matofali kutokana na kukaidi amri aliyompa.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ahmed Msangi

Katika tukio la kwanza mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Mwashiwawala wilaya ya Mbeya vijijini mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la Dickson Kawawa (50) ameuawa kwa kupigwa kwa vipande vya matofali na mtoto wake kwa madai ya kukaidi amri aliyopewa na mtoto huyo ya kuacha kunyuwa pombe.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amesema mtoto huyo aliyefahamika kwa jina Siku Dickson (20) alifanya tukio hilo jana majira ya saa 18:00 jioni katika kijiji cha Mwashiwawala, ambapo mtuhumiwa huyo alimpiga na mawe baba kulikopeleka kutokwa damu nyingi na Kusababisha kifo chake.

Kamanda Msangi amesema katika tukio la pili Mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Jangurutu wilaya ya Mbarali aitwaye Jailos Goyage (56) amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T. 888 BRD, aina ya Toyota Land Cruiser ikiendeshwa na dereva aitwaye Omary Nuru (36) mkazi wa mpakani Ubaruku.

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 15.10.2015 majira ya saa 20:00 usiku huko kijiji cha Jangurutu, kata na tarafa ya Rujewa, wilaya ya Mbarali, mkoa wa Mbeya huku akibanisha kuwa chanzo cha ajali ni mwendo kasi dereva amekamatwa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wanafamilia kutatua migogoro yao kwa kukaa meza ya mazungumzo.

Aidha anatoa wito kwa madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria/michoro na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.