Jumanne , 6th Oct , 2015

Mashindano makubwa ya kucheza Afrika Mashariki ya Dance 100% 2015, yanatarajia kufikia kilele chake siku ya jumamosi ya tarehe 10/10/2015, na mshindi kujinyakulia kitita cha shilingi milioni tano za kitanzania, pamoja na zawadi nyingine.

Akiongea na mwandishi wa habari mratibu wa mashindano hayo ambayo yanaratibiwa na East Africa Television na East Africa Radio Happy Shame, amesema maandalizi ya fainali hizo tayari yamekamilika na yatakuwa ya tofauti kubwa na miaka ya nyuma.

"Mwaka huu mashindano yatakuwa na tofauti sana, kuna magroup ambayo yameingia fainali ambayo tayari yalishaingia kwenye mashindano yaliyopita, kwa hiyo ushindani utakuwa mkubwa sana yani kila mtu anamuogopa mwenzake, na cha pili fainali za miaka yote tulikuwa tunafanyia kwenye viwanja vya basket ball, sasa hivi kuna stage, ambayo ni sehemu ambayo kila mtu anawaona", alisema Happy.

Pamoja na hayo Mratibu huyo amesema kwenye fainali hizi wameongeza majaji na kufikia watano, ili kuleta utofauti katika kukua kwa mashindano hayo.

"Tumeamua kufanya hivyo ili kuweka tofauti alafu tuone hawa majaji watatu walikuwepo toka kwenye mchujo mpaka robo fainali, kwa hiyo tukasema tuweke majaji wengine tuone wao wanaona nini kwa hawa madancer, kwa hiyo tukaongea na watu wa BASATA ambao ndio wanatusimamia, na madancers wenyewe na majaji wa zamani wakasema sawa, na hii yote ni kujua kwamba mchezo unakuwa", alisema Happy.

Pia Happy ameyataka makundi ambayo yalishiriki lakini hawakufanikiwa kufika fainali, waitumie nafasi hiyo kuzidi kujitangaza na kuweza kujipatia ajira, kupitia sanaa hiyo ya kucheza.