Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), marehemu Mchungaji Christopher Mtikila.
Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party, mchungaji Christopher Mtikila amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea mapema asubuhi leo maeneo ya Chalinze mkoa wa Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Jaffary Mohammed amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kwamba marehemu amefariki baada ya gari yake aliyokuwa akisafiria akitokea mkoani Morogoro kuja jijini Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.
Kwa mujibu wa Kamanda Mohammed, ajali hiyo imetokea majira ya saa kumi na mbili kasorobo katika kijiji cha Msolwa karibu na Chalinze na kwamba abiria wengine watatu waliokuwemo kwenye gari hiyo nao wamejeruhiwa na wamekimbizwa hospitali ya tumbi Kibaha kwa matibabu zaidi.
Mchungaji Mtikila atakumbukwa kwa misimamo yake juu ya haja ya kutaka kutambulika kwa taifa la Tanganyika, suala la mgombea huru pamoja na harakati nyingine nyingi za kisiasa ambapo mara kadhaa alijikuta akiingia katika msuguano na vyombo vya dola na hata kufikishwa mahakamani.
Mungu Ailaze Roho ya Mchungaji Christopher Mtikila mahali Pema Peponi—Amen.