Alhamisi , 10th Sep , 2015

Serikali imetangaza kuongezeka kwa wakimbizi kutoka nchini Burundi na kufikia 91, 661 ambao kwa sasa wamehifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.

Taarifa hiyo imetolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambayo imeeleza kwamba tangu waanze kuingia mwezi aprili mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine, imekuwa ikiwapokea na kuwapa hifadhi na huduma nyingine ikiwemo malazi, ulinzi, chakula, maji, elimu na afya.

Taarifa hiyo imesema kwamba kutokana na kuboreshwa na kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama katika kambi ya Nyarugusu, kumesaidia kudhibiti kwa magonjwa ya mlipuko na kukabiliana na magonjwa yasiyo ya mlipuko kambini hapo.