Alhamisi , 10th Sep , 2015

Timu ya Taifa ya soka ya wanawake imetupwa nje ya michuano ya Afrika baada ya kufungwa na Nigeria ‘Super Falcons’ mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi A inayoendelea Kongo Brazzaville.

Kipigo hicho cha Nigeria Inayofundishwa Christopher Musa Danjuma kinakuwa cha pili kwa Tanzania, baada ya awali kufungwa 1-0 na Ivory Coast katika mchezo wa kwanza hivyo kuishia hatua ya makundi.

Super Falcons sasa inajihakikishia kwenda Nusu Fainali za michuano hiyo kwa pointi zake sita baada ya kuwafunga wenyeji Kongo 5-1 katika mchezo wa kwanza.

Mchezo mwingine wa kundi hilo uliwakutanisha Kongo na Ivory Coast ambapo Ivory Coast iliwachapa wenyeji bao 1-0.
Nigeria itamaliza na Ivory Coast, wakati Tanzania na Kongo wakimalizia michezo yao ya mwisho ya makundi huku wakiwa wamepoteza michezo miwili.

Kikosi cha Nigeria kilikuwa; Oluehi Tochukwu, Edoho Blessing, Osinachi Marvis Ohale, Osarenoma Igbinovia, Onome Ebi, Gladys Akpa, Wogu Chioma Success, Ugochi Desire Oparanozie, Ukpong Esther Sunday, Adeboyejo Yetunde Oluwatosin na Nwabuoku Evelyn Chiedu.

Tanzania; Fatuma Omar Jawadu, Anastas Katunzi, Stumai Athumani, Amina Bilal, Fatuma Issa Maonyo, Donisia Minja, Mwanahamisi Shurua, Happyness Hezron, Fatuma Salum, Asha Rashid na Sophia Mwasikili.