Alhamisi , 6th Aug , 2015

Mamlaka ya Ustawishaji makao makuu (CDA) imewataka wakazi wa mji wa Dodoma kuepukana na matapeli wanapotaka huduma mbalimbali ndani ya mamlaka hiyo kwani wengi wao hutoa huduma kwa gharama kubwa huku mamlaka hiyo ikitoza gharama kidogo kwa huduma

Muonekano wa Mji wa Dodoma ambao unasimamiwa na CDA

Akizungumza na East Africa Radio kwenye viwanja vya maonyesho ya wakulima na wafugaji nanenane yanayofanyika kanda ya kati katika viwanja vya Nzuguni Mjini Dodoma, Ofisa Habari wa CDA, Angela Msimbila amewataka wananchi hao kupata huduma wanazozihitaji ndani ya ofisi za mamlaka na si vinginevyo.

Amesema kumekuwa na baadhi ya wafanya kazi ambao siyo waaminifu ambao hutumia mwanya wa kufanya kazi katika mamlaka kwa ajili ya kujipatia kipato kinyume na taratibu ambao hutoza gharama kubwa kwa huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo na kuchafua sifa ya utendaji wa CDA.

Amesema kuwa maonyesho hayo yanatoa wigo mpana kwa wananchi kuelewa kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo kwani hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote.