Jumatatu , 8th Jun , 2015

Serikali ya Tanzania leo imesaini mkataba wa fedha za Tanzania zaidi ya shilingi bilioni miambili kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya maliasili katika mikoa ya kanda ya kusini nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Lazaro Samwel Nyalandu.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mh Lazaro Nyalandu amesema mktaba huo ni wa kwanza kwa ukubwa kuwahi kusainiwa na benki ya dunia katika sekta ya utalii barani Afrika na kwamba utasaidia kuchochea maendeleo kwa vijana na wakazi wa mikoa ya Kusini.

Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu, kusainiwa kwa mkataba huo kutasaidia kuwepo kwa usawa wa kimaendeleo unaotokana na sekta ya utalii kwani wananchi wa mikoa ya Kusini hivi sasa watakuwa na fursa sawa kama walizopata wenzao wa mikoa ya Kaskazini.

Sehemu kubwa ya fedha hizo kwa mujibu wa Waziri Nyalandu zitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa hoteli za kisasa pamoja na aina nyingine za miundombinu ambayo itachochea ukuaji wa utalii katika mikoa ya Kusini.

Waziri Nyalandu amesema hiyo ni fursa muhimu kwa vijana wa mikoa hiyo ambao amesema hivi sasa wanatakiwa kujiandaa kuchangamkia fursa za kiuchumi kwa kusomea fani zitakazowasaidia kuajiriwa katika sekta ya utalii na kufungua biashara zitakazonunuliwa na watalii watakaotembelea maeneo yao.

Aidha, amewataka wakulima nao kujiandaa kuongeza ubora wa mazao wanayoyalima ili yafikie viwango vya kutumiwa na watalii, hatua aliyodai kuwa itasaidia kukuza pia sekta ya kilimo na maisha ya wakulima wa mikoa hiyo.