Jumatano , 13th Jul , 2022

Klabu ya Simba imefanikiwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji Augustine Okrah kutoka Bechem United inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ghana kwa mkataba wa miaka miwili.

Augustine Okrah

Nyota huyo aliyeonyesha kiwango kizuri msimu ulioisha akiwa na timu hiyo unakuwa ni usajili wa tatu kwa wachezaji wa kigeni baada ya kuwatambulisha Moses Phiri kutoka Zanaco ya Zambia na Victor Akpan aliyekuwa anaichezea timu ya Coastal Union.

Mbali na usajili huo kwa wageni ila wapo wazawa wawili waliotambulishwa na kikosi hicho chini ya kocha wake, Zoran Maki ambao ni Mshambuliaji, Habib Kyombo aliyetoka Mbeya Kwanza na nyota mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani Nassoro Kapama kutoka Kagera Sugar.

Katika Ligi ya Ghana Okrah amehusika kwenye mabao 17 akiwa na Bechem ambapo amefunga 14 na kutoa pasi (Assisti) tatu katika michezo 31 aliyocheza huku akitarajiwa kuungana na kikosi hicho kinachoelekea Misri kesho kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Okrah ameitumikia timu ya taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2013 ambapo mwaka 2019 aliitwa kwa mara ya kwanza timu ya taifa ya wakubwa ya Ghana.