Jumamosi , 16th Jul , 2016

Shirikisho la Soka Tanzania TFF limewataka viongozi wa soka wa mikoa nchini kuzingatia umuhimu wa mashindano ya vijana chini wa umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars.

Katibu mkuu wa TFF Mwesingwa Celestine amesema, viongozi wengi wa mikoa wamekuwa wakiondoa lengo hasa la mashindano hayo la kukuza vipaji vya vijana na badala yake hutafuta matokeo bila kujali vipaji.

Mwesingwa amesema, miradi ya kukuza soka la vijana ndio njia pekee ya kukuza soka sehemu yeyote duniani hivyo viongozi wa soka wanatakiwa kufuatilia na kutii sheria na kanuni ambazo zinaongoza michuano ya Airtel Rising Stars.

Michuano ya Airtel Rising Stars inatarajiwa kuanza mwishoni mwezi huu katika ngazi ya mkoa na kufikia ukingoni Agosti 28 huku fainali za Taifa zikichezwa Dar es Salaam Septemba 6 mpaka 11 2016.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde alisema michuano ya Airtel Rising Stars 2016 ni fursa nyingine kwa vijana kuonyesha vipaji vyao vya soka na kupata nafasi ya kutimiza ndoto zao.

Matinde aliongeza kuwa Airtel Rising Stars 2016 imeungana na promosheni ya Airtel Tanzania maarufu kama ‘Airtel Fursa’ ambayo inalenga kusaidia vijana wenye miradi yao ya maendeleo ambayo imeshindwa kupata Mafanikio kwa kukosa mitaji.

Michuano hiyo kwa mwaka itashirikisha mikoa ya Mwanza, Morogoro, Mbeya, Temeke, Ilala na Morogoro kwa wavulana na Ilala, Kinondoni, Temeke, Lindi, Zanzibar na Arusha kwa wanawake ambapo usajili kwa wachezaji watakaoshiriki michuano hiyo unatarajiwa kuanza Jumatatu ya Julai 18 mwaka huu.