Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro'
Gor Mahia ya Kenya imeondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga ya Tanzania Bara Katika mchezo rasmi wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Kagame uliopigwa katika dimba la taifa jijini Dar es salaam.
Magoli ya Gor Mahia yamefungwa na Haron Shakava dakika ya 16 na Michael Olunga dakika ya 46 wakati la Yanga likipatikana dakika ya 5 baada ya beki wa Gor Mahia Glay kujifunga kutokana na krosi iliyopigwa na Donald Ngoma.
Donald Ngoma alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 24, wakati Nadir Haroub Canavaro akikosa mkwaju wa penati dakika ya 73, penati iliyopatikana baada ya mchezaji mmoja wa Gor Mahia kuunawa mpira katika eneo la hatari.
Katika uwanja wa Karume, KMKM ya Zanzibar imeifunga Telecom ya Djibout bao 1-0, na katika mechi ya kwanza APR ya Rwanda imeifunga Al Ahly Shandy ya Sudan bao 1-0.
Michuano hiyo itaendelea kesho ambapo katika uwanja wa Karume LLB AFC ya Burundi itacheza na Heegan FC ya Somalia saa 10:00 jioni, Adama City ya Ethiopia itacheza na Malakia ya Sudani Kusini kuanzia saa 8:00 mchana uwanja wa Taifa na Azam FC ya Tanzania Bara itacheza na KCCA ya Uganda saa 10:00 jioni uwanja wa Taifa.
Michuano hiyo imefunguliwa na waziri wa ujenzi Dkt John Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi akiongozana na aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga.