Jumatano , 2nd Apr , 2014

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga SC, wamelishutumu shirikisho la soka hapa nchini TFF na bodi ya ligi kwa kufanya mipango ya makusudi kuisaidia Azam itwae ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara.

Baraka Kizuguto-Afisa Habari wa Yanga SC

Afisa habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto amesema kitendo cha TFF na bodi ya ligi kubadilisha ghafla ratiba ya ligi kuu ni mbinu ya wazi ya kuwafanya Azam wajue matokeo ya Yanga ili waweze kuzichanga karata zao vizuri.

Bodi ya ligi imefanya mabadiliko madogo kwenye ratiba ya ligi kuu kwa kuusogeza mbele mchezo kati ya Azam FC na Ruvu Shooting kutoka Jumapili ya tarehe 6 mwezi huu mpaka Jumatano ya tarehe 9 mwezi huu, siku ambayo Yanga watakuwa wanacheza mechi yao ya kiporo dhidi ya Kagera Sugar.

Sababu ya mabadiliko hayo ni kwamba Azam ina wachezaji watano kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) ambayo kesho tarehe 3 itaenda Kenya kwa mchezo wa kufuzu mataifa ya Afrika dhidi ya wenzao wa huko utakaofanyika tarehe 6 mwezi huu.