Jumatano , 14th Jul , 2021

Klabu za Simba na Azam zitakosa huduma ya wachezaji wake muhimu katika mechi yao ya kesho ambao ni muendelezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.

Mshambuliaji wa Simba, Medie Kagere akijaribu kufunga bao dhidi ya kipa wa Azam, Mathias Kigonya kwenye mchezo wa VPL duru la kwanza uliomalizika kwa sare ya 2-2.

Mabingwa Simba wao watakosa huduma ya winga wake Benard Morrison mwenye matatizo ya kifamilia,Miraji Athumani na Ibrahim Ajibu wote wanaougua Malaria huku Jonas Mkude akiwa bado sakata lake la utovu wa nidhamu likiwa halijatolewa hatma yake.

Kwa upande wa Azam Fc itaendelea kumkosa mshambuliaji wake kinara Prince Dube ambaye hajapona majeraha yake, Aggrey Morris na Salum Aboubakar ''Sure boy'' ambao wote wanaugua Malaria.

Mchezo wa kesho ni wa heshima kwa wekundu wa msimbazi ambao tayari wameshatwaa ubingwa wakiwa na alama 79, huku Azam wao wakihitaji ushindi katika mechi zote zilizosalia ili wafikishe alama 60 huku wakiwaombea Yanga wenye alama 70 wafungwe michezo yote ili wao wakamate nafasi ya pili katika msimamo ambao utawafanya washiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.