Ijumaa , 8th Jul , 2016

Wanawake wametakiwa kujitokeza kwa wingi zaidi kwa ajili ya kusomea kozi ya mchezo wa mpira wa meza kwa ajili kukuza mchezo huo kwa watoto wa kike mashuleni.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kozi ya ukocha wa mpira wa Meza wakiwa darasani.

Akizungumza na East Africa Radio, mmoja wa washiriki wa kozi ya ukocha wa mpira wa meza daraja la pili yanayotambuliwa Shirikisho la Mpira wa Meza Duniani ITTF Neema Mwaisyula amesema, wanawake wanatakiwa kujitahidi kutumia fursa wanazozipata kwa ajili ya kujiendeleza kimichezo ili kuweza kupata walimu wengi wa kike wa michezo ambao pia watakuwa na uwezo wa kuendeleza zaidi mchezo huo hapa nchini.

Neema amesema, wanawake wengi wamekuwa wakijirudisaha nyuma pamoja na kukata tamaa katika suala zima la michezo bila kujua kuwa wanauwezo mkubwa wa kuendeleza michezo hapa nchini.

Kwa upande wake Yahya Mungilwa ambaye pia ni mshiriki wa kozi hiyo amesema, mafunzo hayo yatatoa muelekeo mzuri zaidi katika mashindano mbalimbali kwani makocha walioshiriki kozi hiyo watakapomaliza watakuwa na uelewa zaidi ya hapo awali kuhusu mchezo huo.

Kwa upande mwingine Mungilwa amevitaka vilabu vya michezo mingine hapa nchini kuanzisha kozi mbalimbali kwa makocha ili kuweza kukuza michezo nchini ikiwa ni pamoja na kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya kimichezo duniani.

Mafunzo hayo yalianza rasmi Julai 04 mwaka huu chini ya Mkufunzi Ahmed Dawlatly kutoka nchini Misri.