Alhamisi , 14th Apr , 2016

Uongozi wa klabu ya Yanga umewakumbusha wanachama wake kulipia kadi za uanachama ili kuongeza kipato cha klabu hiyo inayotumia zaidi ya milioni 90 kuendesha klabu kila mwezi.

Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro amesema kuna wanachama wamekuwa watu wa kulalamika, kuwa klabu hiyo inazuia mechi zake za kimataifa kuonyeshwa kwenye Luninga, lakini hiyo yote inatokana na wao kutokukubali kulipwa kidogo na wanunuaji wa haki za matangazo, hivyo kama wanachama wangelipia kadi zao wangewaonyesha mpira.

Aidha Muro amesema kwa sasa wanapata milioni 35 kila mwezi kutoka kwenye udhamini, kiasi ambacho hakikidhi na gharama wanazotumia ikiwa ni milioni 90 kwa mwezi, lakini kama wanachama wangelipia kadi wangekusanya fedha nyingi, na ingetosha kuendesha klabu kwa kulipa mishahara, usafiri, malazi na mengineyo.

Yanga iliruhusu mechi iliyopita dhidi ya Al Ahly kuonyeshwa kwenye Luninga moja hapa nchini, lakini ilikataa mechi zake za awali dhidi ya APR na Cercle de Joachim kuonyeshwa.