Jumamosi , 9th Jan , 2016

Wachezaji wa kitanzania wametakiwa kutambua umuhimu wao na thamani ya Soka ili kuweza kufikia malengo zaidi kama aliyoyafikia hivi sasa mshambuliaji wa Kimataifa Mbwana Ally Samatta.

Kocha Msaidizi wa Mbeya City Juma Mwambusi amesema, Samatta ni mchezaji wa kuigwa kutokana na kujitambua kwake na kuthamini kazi yake hivyo vijana wanatakiwa kuwa na wivu wa kimaendeleo kupitia kwa Samatta.

Mwambusi amesema, Samatta amezidi na atazidi kuitangaza Tanzania katika ramani ya soka kutokana na mafanikio yake yaliyosababishwa na nidhamu pamoja na uvumilivu katika kazi yake hivyo vijana wanatakiwa kuiga mfano wake ili kufika mbali zaidi na kupata wakina Samatta wengi zaidi.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Simba Hajji Manara amesema, Samatta ameonesha matunda ya kujituma na kujitambua na kukipata alichokikusudia hivyo wachezaji watanzania wanatakiwa kucheza kufika alipo au zaidi ya Samatta ili kuzidi kufika mbali zaidi.

Manara amesema, Tanzania kuna vipaji vingi vya mpira lakini vijana wenyewe bado hawajajitambua suala linalochangia kwa vijana hao kushindwa kufikia malengo.

Manara amesema, Shirikisho la Soka nchini TFF pia linatakiwa kuangalia au kuandaa program itakayosaidia kuwakuza vijana katika michezo na kuweza kufikia malengo ya muda mrefu yakuwa na wachezaji wengi wa kimataifa kama zilivyo nchi nyingine.