Ijumaa , 16th Mar , 2018

Wachezaji wa Simba wametakiwa kukumbuka baadhi ya mechi ambazo klabu hiyo imewahi kushinda dhidi ya timu za Uarabuni na kusonga mbele kwenye mashindano ya kimataifa.

Rai hiyo imetolewa na mkuu wa kitengo cha habari wa klabu hiyo Haji Manara kwa lengo la kuwakumbusha wachezaji kuwa kila kitu kinawezekana kuelekea mchezo wao wa marudiano wa Kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri.

''Najua mnaweza, mshafanya hivyo mara kadhaa ugenini, hakuna asiyejua mlichofanya kwa Zamalek, Al Ahly, Setif, Al Harach na wengine kadhaa, lindeni heshma ya Simba na Taifa kwa ujumla'', ameandika Manara kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Baada ya kumtafuta Manara amefafanua kuwa ''lengo ni kuwakumbusha tu na kuwapa moyo vijana wetu, muda mwingine wanaweza kuwa wanahisi haiwezekani kumbe ilishafanyika hivyo mara nyingi tu''.

Simba itashuka dimbani Jumamosi hii huko Port Said Misri kuivaa Al Masry ikiwa inahitaji ushindi baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam.