Jumanne , 12th Oct , 2021

Wachezaji sita wa kikosi cha kwanza cha Simba waliopata majeraha wiki mbili zilizopita wamepona na wameanza mazoezi ya pamoja ili wacheze dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana kuwania kufuzu makundi Klabu bingwa Afrika.

Wacheza wa Simba wakiwa kwenye mazoezi ya pamoja.

Wachezaji hao ni mlinzi wa kati Joash Onyango na kiungo Sadio Kanoute, Onyango aliumia kichwani wakati Kanoute aliumia mguu kwenye mchezo wa fainali ya Ngao ya Hisani ya Jamii dhidi ya Yanga Septemba 25, 2021.

Onyango yupo fiti kwani alijumuishwa kwenye kikosi cha timuya taifa ya Kenya kwenye michezo miwili ya kuwania kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Mali na Rwanda wakati Kanoute alisalia nchini kufanya mazoezi na kambi ya Simba.

Mlinzi wa kulia aliyeumia kwenye mchezo dhidi yaBiashara United Mara Septemba 28, 2021, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni aliyeumia mazoezi wawili hawa nao wamerejea kikosini na wamefanya mazoezi na wenzao.

Wachezaji wengine ambao wamerejea kwenye utimamu wao ni mlinzi wa kati Kennedy Juma na winga Pape Ousmane Sakho ambao walioumia wote kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Dodoma Jiji Oktoba 1, 2021 na kushindwa kuendelea na mchezo huo.

Kennedy Juma aliyepigwa kiwiko na mchezaji wa Dodoma Jiji, Anuary Jabir, aliitwa kwenye mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Benin  Oktoba 10, 2021 na kuonesha kiwango safi huku Sakho alisalia na kambi ya Simba tokea wiki iliyopita.

Kurejea kwa wachezaji hao pamoja na mshambuliaji wa Kibu Denis kupata vibali vya kuchezea Simba akiwa raia wa Tanzania, vitawafanya wekundu hao wa msimbazi wawe na machaguo mengi kuwavaa Galaxy Jumapili ya Oktoba 17, 2021 kuwania kufuzu hatua ya makundi michuano ya klabu bingwa Afrika