Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu, jana hakufanya mazoezi na timu ya taifa, Taifa Stars kwa sababu ya maumivu ya mguu.

Ulimwengu baada ya kuwasili na wachezaji wenzake Uwanja wa Taifa, alijaribu kufanya mazoezi ya awali ya kuamsha misuli kidogo na kushindwa kuendelea hadi akatolewa nje.

Madaktari wa Taifa Stars walijaribu kuhangaika naye kumrejesha uwanjani, lakini hakuweza kabisa kurudi mazoezini.

Daktari Mkuu wa Taifa Stars, Gilbert Kigadye alisema Ulimwengu aliumia juzi akifanya mazoezi na jana ameshindwa kabisa kuendelea na mazoezi.

"Tunachofanya hapa ni kumpatia tiba ya kuondoa maumivu na kumpumzisha ili pate ahueni, si maumivu makubwa, aligongwa kidogo tu,” alisema Dk. Kigadye.

Taifa Stars inatarajiwa kumenyana na Misri kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kundi G kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.