Ijumaa , 25th Mei , 2018

Mshambuliaji wa Tanzania  Thomas Ulimwengu, ameachana na soka la Ulaya baada ya kumalizana na klabu ya AFC Eskilstuna ya Sweden aliyokuwa akiitumikia na kujiunga na timu ya El Hilal ya Sudan.

Ulimwengu anarejea uwanjani baada ya kupona maumivu ya goti kufuatia kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.

Maumivu ya goti yamekuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza.

Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.

Hat hivyo bado haijafahamika ni mkataba wa muda gani amesaini na timu hiyo ya Sudan. El Hilal ni moja ya timu bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na imekuwa ikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataia.