Kwa mara ya kwanza baada ya kizazi cha Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Sergio Busquets, Victor Valdes, Gerald Pique na Carles Puyol Barcelona imeanza na Wachezaji Watano kutoka kwenye kituo cha kulelea Wachezaji cha La Masia kwenye dimba la Santiago Bernabeu mchezo wa El Clasico dhidi ya Real Madrid.
Jana usiku uwanja wa Santiago Barnabeu ulichezwa mchezo wa El Clasico uliozikutanisha timu mahasimu wakubwa nchini Hispania Real Madrid dhidi ya Barcelona. Barca ilipata ushindi wa goli 4-0 huku wakicheza mchezo wa kuvutia na kuwatawala Wenyeji wao kwa kiasi kikubwa.
Hansi Flick Kocha wa Barca raia wa Ujerumani alianza na Wachezaji Watano kutoka kwenye kituo cha kuzalisha Wachezaji cha La Masia kinachomilikiwa na klabu hiyo kutoka Catalunya. Muda mrefu mafanikio ya Blaugrana yametokana na vipaji vilivyopandishwa timu ya Wakubwa tokea kwenye kituo chao cha La Masia.
Xavi Hernadez, Andres Iniesta, Lionel Messi na Sergio Busquets walitawala soka la Ulaya na Hispania zaidi ya miaka 10 na wao wote ni faida kutokana na uwekezaji uliofanyanyika kwenye Akademi yao. Marais waliopita ndani ya klabu yenye kubeba utambulisho wa Watu wa Catalunya Sandro Rosell na Josep Maria Bartomeu waliachana na utamaduni wa Blaugrana na walisajili Wachezaji ambao hawakuleta tija kwenye kikosi hiko na kupoteza utambulisho wake pamoja na utawala wao wa soka Ulaya.
Joan Laporta aliporejea kuwa Rais wa Barcelona kwa awamu ya pili aliikuta timu ikiwa na wakati mgumu kiuchumi na Lionel Messi aliondoka kwenda kujiunga na PSG mwaka 2021. Laporta alibidi atafute njia mbadala ya kuijenga timu mpya shindani huku timu ikiwa haina uwezoa wa kusajili kutokana na ukosefu wa fedha.
Alimrudisha kikosini Anderson Luís de Souza maarufu kwa jina la Deco kwenye nafasi ya Ukurugenzi wa ufundi wa klabu kwa pamoja wakarejesha matumaini yao kwa kuangalia vipawa kutoka kituo chao cha soka ili kujenga timu pasipo kuongeza gharama ya matumizi. Wakaamua kupandisha kikosi cha kwanza Wachezaji ambao wanaonekana wana ubora wa kuitumikia timu ya Barcelona.
Lamine Yamal, Pau Cubarsi, Fermin Lopez, Marc Casado, Gavi , Aljando Balde na Ansu Fati walipandishwa timu ya Wakubwa na kuanza kutumika kwenye kikosi cha kwanza. Mchakato ulianza na Ronald Koeman na Xavi Hernandez kwa sasa upo chini ya Hansi Flick. Ulikuwa ni mpango ambao haukuungwa mkono na Mashabiki wa Barcelona lakini kutokana na maono ya Rais Joan Laporta kwa sasa Barca inauwezo wa kushindana kwenye mashindano makubwa na kucheza na timu zenye Wachezaji wenye uzoefu bila shida yoyote.
Tulichokishuhudia usiku wa jana kwenye dimba la Santiago Bernabeu ni mwanzo wa utawala mpya wa Barcelona kwenye soka la Hispania pamoja na Ulaya, Wachezaji waliokulia kwenye kituo maarufu cha kukuza vipaji cha La Masia Wameonyesha wanauwezo wa kucheza uwanja wowote na kupata matokeo ya ushindi huku ile falsafa ya soka la Tiktaka ikionekana.
Joan Laporta amefanikiwa kuifufua La Masia na kituo hiko kimeifufua Barcelona, Wachezaji Watano wote wamezaliwa miaka ya 2000 walianza kwenye mchezo wa El Clasico na kuwatawala Wenyeji wao bila uwoga wowote. Rasmi sasa utawala mpya wa Blaugrana umerejea na La Masia imeanza kuzalisha upya vipaji ambavyo vitaweza kutawala soka kwa la Hispania na Ulaya kwa miaka kumi ijayo.