Jumanne , 7th Apr , 2015

Uchaguzi wa Chama cha mchezo wa Gofu nchini TGU unatarajiwa kufanyika Mei mwaka huu jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Rais wa TGU nchini, Joseph Tango amesema wagombea wote wenye sifa za kugombea wameshachukua fomu za kugombea katika nafasi mbalimbali za chama hicho huku fomu hizo zikitakiwa kurudishwa mwishoni mwa mwezi huu.

Tango amesema, nafasi za ugombea katika chama hicho ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu mkuu, Muweka hazina na katibu wa mashindano.

Tango amesema, katika Uchaguzi huo kwa kila mgombea wameangalia vigezo ambavyo ni lazima vizingatiwe vikiwemo kila mgombea kuwa mchezaji wa Gofu na awe amechaguliwa na Kapteni wa klabu yake huku kwa upande wa Mwenyekiti na makamu mwenyekiti wanatakiwa wawe wamefanya jambo lolote la kuleta maendeleo katika mchezo wa Gofu iwe katika klabu au Chama.