Jumatatu , 21st Mar , 2016

Timu za taifa za soka za wanawake Twiga stars na ile ya wanaume ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys wamebadilishana kambi ya mazoezi zilizopo katika ofisi za makao makuu ya Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF.

Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya wanawake Tanzania Twiga Stars.

Unaweza kusema timu hizo zimebadilishana kambi kwa kuwa hii leo wakati timu ya soka ya taifa ya wanawake Twiga Stars iliyowasili kutoka Zimbabwe ambako ilitupwa nje na wenyeji wao Zimbabwe katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Afrika kwa jumla ya mabao 3-2 wao walirejea nchini alfajili ya leo na kupumzika katika kambi hiyo kwa muda mfupi na baadae kila mmoja kutawanyika kwenda makwao.

Wakati Twiga wakiondoka katika kambi hiyo wenzao Serengeti boys wao wameanza kambi katika eneo hilo hilo wakijiwinda na mchezo wa kwanza dhidi ya Shelisheli wakuwania kucheza fainali za michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 itakayofanyika nchini Madagascar mapema mwakani.

Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Zimbabwe uliopigwa huko Harare na kuishia kwa sare ya bao 1-1 na hivyo Tanzania kutupwa nje ya michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wanawake kocha msaidizi wa timu ya Twiga Stars Edna Lema amesema pamoja na ubora wa wachezaji wa timu hiyo bado suala la kukosa uzoefu ndilo limekuwa kikwazo kwao sababu kubwa ikiwa ni kukosekana na kwa ligimbalimbali za wanawake nchini na pia mashindano ya mara kwa mara na hata timu hiyo kukosa michezo ya kirafiki ya kujipima uwezo na timu za wanawake zilizokatika viwango vya juu katika viwango vya ubora Afrika na duniani kwa ujumla

Akimalizia Lema ametoa wito kwa wadau mbalimbali makampuni kuhakikisha wanasaidia kwa hali na mali ili kuinua soka la wanawake kwani kwa uwezo ulioonyeshwa na timu hiyo ambayo haikuwa na udhamini wala maandalizi yakutosha ni wazi wakiwezeshwa wataliletea sifa taifa katika medani ya kimataifa.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys Bakar Shime amesema hivi sasa ni wakati wa Watanzania kujitolea kwa hali na mali kulisaidia shirikikisho katika kuziwezesha timu za vijana kufanya maandalizi mazuri na kuweza kufuzu ama kushinda mashindano wanayoshiriki.

Shime amesema kuziwezesha timu za vijana ambazo ni timu za wakubwa za kesho ni faida kubwa katika michezo kwa baadae kwani vijana hao waliopo sasa ndiyo wanataraji wa kuwa timu ya taifa ya baadae hivyo kuwekeza kwao ni njia sahihi hasa ikizingatiwa nchi zote zilizofanikiwa dunia kote ziliwekeza kwa vijana ambao sasa wanazitangaza vema nchi zao katika medani ya mimataifa.