Ijumaa , 4th Mar , 2016

Timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars imeshindwa kufurukuta mbele ya wazimbabwe baada ya kutandikwa bao 2-1 hii leo Uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam katka kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake baadaye mwaka huu Cameroon.

Twiga Stars walitangulia kupata bao kupitia kwa kiungo wake mahiri, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 18 kwa shuti kali la mbali baada ya kupokea pasi ya Asha Rashid ‘Mwalala’.

Zimbabwe waliweza kutumia nafasi waliyoipata ndani ya dakika tatu na kuchomoa bao hilo baada ya Erina Jeke kusawazisha kwa shuti la mbali dakika ya 19.

Mwanahimisi Gaucho alipata nafasi dakika ya 39 lakini hakufanikiwa kuleta madhara katika lango la Zimbabwe na hatimaye mpira kutoka na kupelekea timu kwenda mapumziko dakika zikiwa zimefungana bao 1-1.

Kipindi cha pili, Twiga Stars inayofundishwa na Nasra Juma ilirudi ikiwa imepoteza matumaini ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo na kuwaruhusu wageni kutawala mchezo huo ambapo katka dakika ya pili ya kipindi cha pili zikiwa ni dakka 47 Erina Jeke alifumua shuti lililomfanya mlinda Mlango wa Twiga Fatuma Omar kuushindwa mpira na kuelekea golini.

Tanzania sasa itabidi ishinde ugenini kwa tofauti ya mabao mawili, au 2-1 ili mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Fatuma Omary, Stumai Abdallah, Maimuna Khamis/Fatuma Khatib dk73, Fatuma Issa, Annastazia katunzi, Donisia Minja, Happinnes Mwaipaja, Amina BIlali, Shlder Boniphace/Fatuma Makusanya dk21, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’.

Zimbabwe; Chido Dzingirai, Felistus Muzingodi, Eunice Chibanda, Sheila makoto, Nobhule Majika, Luntet Mutokuto, Daisy Kaitano/Rejoice Kapfuvuti dk75, Emmaculate Msipa, Majory Nyauwe, Erina Jeke/Mavis Chirandu dk79 na Rudo Neshamba/Patience Mujuru dk90