Jumatano , 25th Feb , 2015

Kocha msaidizi wa Timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars Edna Lemma amesema anaamini kikosi chake ni bora na kitaweza kuitetea nchi katika mechi yao ya kufuzu Mataifa Afrika dhidi ya Zambia itakayochezwa kati ya Machi 21 na 22 mwaka huu Lusaka Zambia

Akizungumza na East Africa Radio, Lema amesema, mazoezi yanayotolewa kwa wachezaji wanaamini wataitoa Zambia kwani kila mchezaji ana kipaji na kila mtu anataka kuitetea nchi yake.

Lema amesema, mpaka sasa ana wachezaji 33 ambapo wanatarajia kufanya mchujo baada ya wiki mbili ili kuweza kupata wachezaji 25 watakaoweza kubaki kambini kwa wiki mbili nyingine kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi hiyo.

Lema amesema, katika mchujo huo wanaamini kwa upande wao watakuwa na kazi kutokana na kila mchezaji kuwa na kipaji ambacho wanaamini kinaweza kuisaidia timu na nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili amesema, kila mchezaji katika kikosi hicho ameitikia mazoezi ili kuhakikisha anapita kwenye mchujo na kuhakikisha anafanya vizuri ili kumshawishi Kocha kumchagua kwenye kikosi cha awali.

Mwasikili amesema, watanzania wanatakiwa wawe wavumilivu kwani ili timu iweze kufanya vizuri inatakiwa kukaa kwa pamoja kwa muda mrefu hivyo wanaamini programu ya kocha itasaidia timu hiyo kufanya vizuri.