
Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema, kuhusu madai ya madai posho ya kambi ya maandalizi ya mchezo wa marudiano ya kuwania kufuzu kombe la mataifa ya Afrika dhidi ya Chad ambayo Chad walijitoa katika mashindano walishaongea na wachezaji na wakaelewana kwani hela wanazotakiwa kulipwa wachezaji wa Stars zinatakiwa kulipwa na Chad.
Lucas amesema, kanuni zinasema kuwa iwapo timu itajitoa katika mashindano ambayo yanafahamika na shirikisho CAF inamaana timu itakuwa imevunja makubaliano ya kuja kucheza mchezo wa marudiano hivyo watatakiwa kulipa gharama za siku ambayo timu imekaa kambini pamoja na gharama za kuwaathiri kisaikolojia wachezaji wa Stars ambao walikuwa wamejipanga kwa ajili ya mchezo huo.
Lucas amesema kuwa taarifa nyingine ambazo bado zinaendelea kusambaa kuwa mara baada ya mchezo wa Taifa Stars na Misri, wachezaji wa Stars hawakulipwa posho yao sio za kweli kwani mara baada ya kumalizika kwa mchezo ule, Rais wa TFF Jamal Malinzi alimuomba kocha wa Stars Charles Boniface Mkwasa kuelekea kambini na wachezaji ambapo walikabidhiwa posho zao.
Lucas amesema, taarifa zanazosambazwa na baadhi ya watu kwa madai ambayo sio ya kweli zinalenga kuharibu wachezaji ambao mwisho wa siku watashindwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.