Jumatano , 13th Apr , 2016

Kocha wa Mwadui FC Jamhuri Kihwelo Julio amevitaka vilabu vilivyoingia katika hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho Tanzania Bara FA kutokuwa na uoga wa ratiba ya michuano hiyo kwa visingizio vya kuwa na mshindano ya Afrika.

Kocha mkuu wa Mwadui Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

Julio amesema vilabu vingi vikubwa vimekuwa vikihitaji matokeo mazuri ili kuhitaji nafasi za kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika suala ambalo linafelisha soka hapa nchini.

Julio amesema, droo iliyochezweshwa hapo jana inatakiwa kufuatwa na kila timu shiriki bila kuwa na uoga na ratiba.

Julio amesema, anaamini ushindi wa kombe la shirikisho Tanzania bara utabakia kwake kwani anaimani ya kuitoa Azam FC na kuweza kuingia katika hatua ya fainali kati ya Yanga au Coastal Union.

Droo ya nusu fainali ya kombe la shirikisho FA CUP ilichezwa hapo jana ambapo Yanga imepangwa kucheza ugenini dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mwadui ikiikaribisha Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex, Mkoani Shinyanga.

Nusu fainali ya kombe la shirikisho Tanzania bara imepangwa kuchezwa Aprili 24 ambapo viongozi wa Yanga na Azam FC wameipinga ratiba hiyo kwani Yanga SC watakuwa na mchezo wa marejeano ugenini nchini Misri Aprili 20 dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa hatua ya mtoano (16 bora) ligi ya mabingwa Afrika huku Azam FC ikitarajia kucheza mchezo wake wa marudiano wa hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho dhidi ya Esperance Aprili 19 nchini Tunisia.