Jumanne , 8th Dec , 2015

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Willie Chiwango aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki na mazishi kufanyika eneo la Buguruni jijini Dar e salaam.

Nembo ya shirikisho la soka nchini TFF

Katika salam zake, TFF inawapa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na kusema kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini, wako pamoja katika kipindi hiki cha maombolezo.

Marehemu Willie Chiwango ni miongoni mwa waandishi wa habari wa michezo wakongwe kabisa, aliambatana na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki michuano ya Mataifa Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.

TFF ilimpa cheti cha heshima marehemu Chiwango katika zoezi la kuwakumbuka na kutambua mchango wa viongozi, wachezaji, waandishi wa habari za michezo waliojitoa katika sekta ya mpira wa miguu nchini.