Jumanne , 19th Dec , 2017

Shirikisho la soka nchini TFF limethibitisha kuwa mfumo wa usajili wa shirikisho la soka la Kimataifa FIFA umetengemaa baada ya kusumbua kwa siku kadhaa na sasa usajili kuendelea kama kawaida.

TFF imesema imefanya jitihada za kuwasiliana na waendeshaji wa mfumo huo walioteuliwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA) ambao makao makuu yao yapo Tunis, Tunisia ili kuziwezesha timu kufanya usajili na hatua hizo zimefanikiwa.

“Mtandao huo kwa sasa upo wazi, hivyo TFF inazitaka timu zote sasa kukamilisha usajili kuanzia pale walipokwama, Timu zinatakiwa kusajili kabla ya Desemba 23, mwaka huu” imeeleza sehemu ya taarifa ya TFF.
Desemba 15, mwaka huu mfumo wa usajili kwa njia ya TMS ulifeli hali iliyosababisha vilabu kushindwa kukamilisha usajili kwa wakati kupitia mfumo huo.

Awali dirisha dogo la usajili nchini lilifunguliwa Novemba 15 na kufungwa Disemba 15, kabla ya jana kufunguliwa tena hadi Disemba 23 ili kuziwezesha timu ambazo zilikuwa hazijakamilisha usajili kufanya hivyo.