Kikosi cha timu ya Yanga.
Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limesema kupoteza mchezo wa awali dhidi ya timu ya Mo Bejaia kutoka Algeria isiwe sababu ya timu hiyo kuanza kugeuziwa kisogo na mashabiki na kuibeza kwani bado inanafasi ya kugeuza matokeo katika mchezo wa marudio hapo baadae.
Afisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema Yanga iko katika hatua ya makundi ikiwa kundi A lenye timu nne na kila timu itacheza michezo sita mitatu ya nyumbani na mitatu mingine ugenini hivyo basi nafasi ya timu hiyo bado iko wazi kwani bado wanamichezo mitano mkononi ukiwemo wa jumanne ya wiki ijayo Juni 28 utakaopigwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya TP Mazembe kutoka DRC.
Aidha Lucas amesema ifike wakati Watanzania [mashabiki] wajitambue na wawe wazalendo kwa taifa lao badala ya kuweka maslai ya vilabu mbele na kuipa nguvu timu hiyo ambayo si tu kuwa ni wawakilishi wa Tanzania bali pia ni wawakilishi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati waliosalia ama kufika hatua hiyo kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.
Akimalizia Lucas amesema ushindi wa Yanga katika hatua ya makundi ya nane bora na kusonga katika nne bora ama nusu fainali ya michuano hiyo na hata kufika fainali hata kama isipotwaa ubingwa wa kombe hilo kutatoa fursa ya nchi kuongozewa idadi ya timu katika michuano hiyo hivyo Tanzania kuwa na mwakilishi zaidi ya mmoja katika michuano hiyo kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Sudan, Misri, DRC na Algeria ambao wao kila msimu wamekuwa wakiingiza timu zaidi ya moja katika michuano ya CAF [klabu bingwa na shirikisho barani Afrika.]