Jumanne , 22nd Nov , 2022

Timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa kuogolea (Tanzanite) imeshinda taji la kanda ya tatu Afrika baada ya kuzishinda nchi nyingine tisa zilizoshiriki katika mashindano hayo.

Tanzanite ilikusanya jumla ya pointi 3,061 katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye bwawa la kuogelea la klabu ya Gymkhana.

Ushindi huo ni wa tatu katika historia ya Tanzanite katika mashindano hayo kwani mwaka 2016, Tanzania ilishinda taji hilo mjini Kigali, Rwanda na mwaka 2017 ililitwaa tena katika mashindano yaliyofanyika hapa nchini.

Tanzania iliwakilishwa na wachezaji 63 katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na kampuni ya uzalishaji wa sukari Kilombero Sugar Company kupitia chapa ya Bwana Sukari.

Kwa mujibu wa matokeo ya michuano hiyo, nafasi ya pili ilikwenda kwa waogeleaji walioiwakilisha shirikisho lililosimamishwa la Kenya ambao waliruhisiwa kufanya bila kutumia jina la nchi yao na kujulikana kwa jina la ‘ Swimmers from Suspended Federation. Waogeleaji hao walikusanya pointi 2,768 ambapo nafasi ya tatu ilikwenda kwa Uganda iliyopata pointi 2,521.50.

Zambia ilimaliza katika nafasi ya nne kwa kukusanya pointi 1,878 huku Afrika Kusini ikimaliza katika nafasi ya tano kwa kukusanya pointi 1,385. 50.

Mashindano hayo yalianza tarehe 16 na kumalizika 19 Novemba, 2022 jijini Dar es salaam.