Jumatatu , 26th Mei , 2014

Taifa Stars na Malawi (Flames) zinapambana kesho (Mei 27 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni.

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa stars

Malawi tayari ipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo wakati Taifa Stars iliyopiga kambi yake Tukuyu mkoani Mbeya inawasili jijini Dar es Salaam kesho (Mei 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ndege ya Air Tanzania.

Hiyo itakuwa ni mechi ya mwisho ya majaribio kwa Taifa Stars kabla ya kwenda jijini Harare kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors). na kocha mkuu wa stars Mholanzi Mart Nooij ndiye aliyeomba timu hiyo kupatiwa mechi hiyo ili kukipima uwezo kikosi hicho ambacho kitakuwa na mtanange huo mgumu na wazimbabwe.

Afisa habari wa TFF Boniface Wambura amesema pamoja na kupeleka maombi kwa timu ya TP Mazembe ili kuwapata washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu lakini mpaka sasa hawajapata majibu na hivyo ni wazi wachezaji hao hawatakuwemo katika mchezo huo huku TFF ikitegemea kuwapata katika mchezo dhidi ya Zimbabwe.

Malawi (Flames) inayonolewa na mchezaji wake wa zamani Young Chidmozi nayo itakuwa inacheza mechi ya mwisho ya majaribio kabla ya kwenda N’djamena kuikabili Chad.