Alhamisi , 8th Jul , 2021

'SPORTS COUNTDOWN' ya East Africa redio inakujia kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa saa moja na robo kuzangazia zile stori kali za kimichezo zilizojiri kwa mfumo wa namba ambazo zinaanza kwa kubeba stori yenyewe.

Nahodha na Mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, Harry Kane akishangilia baada ya kufunga bao la ushindi na kutinga fainali ya EUROS kwa mara ya kwanza kwenye historia na kuwatupa nje Dernmark kwa 2-1.

Na hii ndiyo 'SPORTS COUNTDOWN' ya leo Julai 8, 2021 na Abissay Stephen Jr.

6 - Ni idadi ya wachezaji ambao kocha wa klabu ya Yanga, mtunisia Mohammed Nasreedin Nabi amepanga kuwasajili kwenye dirisha kubwa la usajili litakalo funguliwa hivi karibuni ili kuendelea kukisuka kikosi hicho cha mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu nchini.

Taarifa za kikachero zinaeleza kuwa miongoni mwa wachezaji hao sita, ni Mlinzi wa kushoto wa KMC David Bryson na winga wa Dodoma Jiji, Dickson Ambundo ambao wamependekezwa na kocha huyo.

5 - Ni idadi za pasi za usaidizi wa mabao alizozitoa nyota wa Argentina Lionel Messi kwenye michuano ya Copa America msimu huu ambapo nyota huyo ameahidi kufanya makubwa wakati timu yake itakapo menyana na mabingwa watetezi wa kombe hilo timu ya taifa ya Brazil saa 9:00 usiku kwenye uwanja wa Maracana nchini Brazil.

4 - Ni idadi ya michezo ya hatua ya robo fainali  michuano ya tenisi ya Wimbledon nchini England, ambapo bingwa mtetezi wa michuano hiyo Mserbia Novak Djokovic amefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kumchapa Marton Fuscovics raia wa Hungary 6-3, 6-4 na 6-4 na kupangiwa kucheza na Denis Shapolov siku ya kesho Julai 9.

Nae bingwa mara 8 wa michuano hiyo, Rodger Federer ametolewa baada ya kufungwa na Hubert Hurkacz 6-3,7-6  na 6-0 na kusema bado hajajua kama michuano ni ya mwisho kwa upande wake kwani kwasasa ana miaka 39 na kuporomoka kiwango.
 
Baada ya Hubert kutiga nusu fainali kwa mara ya kwanza, atacheza dhidi ya Matteo Berrettini siku ya jumapili tarehe 11.

3 - Ni idadi ya mabao yaliyofungwa kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili ya michuano ya UEFA EUROS ambapo timu ya taifa ya England imeifunga Dernmark mabao 2-1 usiku wa kuamkia leo kwenye mchezo ulioamuliwa ndani ya dakika 120 na kufuatia sare ya bao 1 ndani ya dk90 na kuwafanya England kufuzu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza kwenye historia vile vile ikiwa ni fainali yao ya kwanza katika michuano mikubwa tokea 1966 walipotwaa Kombe la Dunia miaka 55 iliyopita.

Dernmark ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Mikkel Damsgaard kwa free-kick kali dk30' na dk ya 39' Nahodha wa Dernmark Simon Kjaer alijifunga na kuisawazishia England na dk104' Harry Kane akaifungia timu yake bao la ushindi kwa kumalizia rebaundi ya kukosa penalti iliyopanguliwa na Kasper Schmeicel wa Dernmark.

Sasa England itacheza dhidi ya Itali kwenye mchezo wa fainali ya michuano hiyo siku ya Jumapili ya Julai 12 mwaka huu kwenye dimba la Wembley.

2 - Ni idadi ya mchezo wa pili katika fainali za NBA unaotaraji kuchezwa alfajiri ya kuamkia kesho Kati ya timu ya Phoenix Suns watakaokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Phoenix Suns Arena kuwakaribisha Milwaukee Bucks huku ikikumbukwa Suns wapo mbele kwa ushindi wa mchezo mmoja baada ya kushinda kwa alama 118-105 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa alfajiri ya kuamkia jana.

Mchezo wa tatu unatazamiwa kucheza tarehe 12 Julai na wanne tarehe 15 Julai mwaka huu.

1 - Ni alama ambayo vinara wa VPL, Wekundu wa Msimbazi Simba inaisaka ili Kufikisha alama 77 ambazo hazitofikiwa na timu yeyote kwenye ligi kuu na kumfanya awe bingwa wa ligi hiyo kwa mara ya nne mfululizo na hii ni mara baada ya kuifunga KMC mabao 2-0 usiku wa jana kwenye dimba la BWM.

Mabao ya simba yamefungwa na mshambuliaji wake wa kimataifa wa DR Congo, Chris Mugalu dakika ya 2' na 44' na kufikisha mabao yake 12 mawili nyuma na Prince Dube na John Bocco wanaoongoza kwa ufungaji.

Baada ya kipigo hiko, KMC wamesalia kwenye nafasi ya 6, michezo 32 wakiwa na alama 42.

Simba itashuka tena dimbani kukipiga na Wagosi wa ndima, timu ya Coastal Union tarehe 11 Juali 2021 saa 1:00 kwenye dimba la Mkapa.