Baadhi ya Mashabiki na wanachama wa Simba wakiangalia moja ya Mechi za timu hiyo
Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Simba ya jijini Dar es salaam nchini Tanzania imewasimamisha uanachama wanachama wake 69 waliokwenda Mahakamani kupinga uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Rais wa Klabu hiyo Evance Aveva amesema hatma ya wanachama hao, pamoja na ya aliyekuwa mgombea wa Urais wa Klabu hiyo Michael Wambura ambaye alienguliwa kwenye uchaguzi kwa kosa kama hilo, itaamuliwa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika Agosti 3, mwaka huu.
Aveva amesema katika kikao hicho pia wameteua kamati mbalimbali katika klabu hiyo zikiwemo kamati ya Soka ya Vijana itakayokuwa chini ya Mwenyekiti, Said Tuliy huku Kamati ya Mashindano Mwenyekiti wake akiwa Mohammed Nassor na kamati ya Usajili ikisimamiwa na Zacharia Hans Poppe.