Jumapili , 24th Apr , 2016

Ni kama wanamfukuza mwizi kimya kimya unaweza kusema hivyo kutokana na kauli ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba Hans Pope akizungumzia mchakato wa kusaka kocha baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu sasa huku kocha Mayanja akiwajibika peke yake.

Pamoja na kocha wa sasa wa timu Simba Mganda Jackson Mayanja kuonekana akifanya vema katika kikosi cha wekundu wa hao Msimbazi lakini bado kumekuwa na taarifa zisizo rasmi kuwa timu hiyo ipo katika mikakati mizito ya kusaka kocha mwingine wa kigeni kuja kukinoa kikosi hicho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema ni kweli wanatafuta kocha wa kufanyakazi pamoja na kocha wao wa sasa, Jackson Mayanja ili kukijenga vema zaidi kikosi hicho ambacho kwa sasa hakina kocha mwingine zaidi ya Mayanja na kocha wa makipa pekee.

Pope ambaye kwa misimu kadhaa amekuwa ndio kama roho ya Simba akisaidia kwa mfuko wake masuala mbalimbali ya timu hiyo hasa katika usajili na hata kambi amesema “Mchakato unaendelea kwa umakini sana na ukimya wa hali ya juu, mambo yakikamilika yatawekwa hadharani” .

Habari za ndani zinasema uamuzi huo unashughulikiwa kwa haraka hasa kutokana na ukweli kuwa kocha Mayanja ameonekana kushindwa kumudu vyumba vya kubadilishia nguo kutokana na migogoro ya mara kwa mara na wachezaji.

Mayanja alianza kwa kutofautiana na beki wa kati wa timu hiyo Hassan Isihaka ambaye alifikia hadi kusimamishwa na uongozi baadaye akatofautiana pia na kiungo Abdi Banda.

Katikati ya mwezi huu akatofautiana na Waganda wenzake, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Hamisi Kiiza, mgogoro ambao hata hivyo ulizimwa kwa busara za uongozi wa timu hiyo na wachezaji hao wako na timu kambini visiwani Zanzibar wakijiwinda na mchezo mgumu na muhimu kabisa wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Azam FC.

“Ni ukweli kwa sasa Simba wanaamini Mayanja ni kocha mzuri na amekuwa sahihi mara zote katika tofauti zake na wachezaji na tangu kutua ndani ya klabu hiyo amefanya marekebisho mengi ikiwemo hata uchezaji wa kuvutia, lakini tu anashindwa kuvumilia mapungufu ya asili ya wachezaji wa Kitanzania, ambayo wanawaambukiza na wageni, ndiyo maana wanamtafutia kocha wa kushirikiana naye atakayerejesha mshikamano baina ya benchi la ufundi na wachezaji,” kwa mujibu wa vyanzo vya ndani.