Jumanne , 5th Apr , 2022

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika Simba SC imepangwa kucheza dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano hii. Na wekeundu wa msimbazi watakuwa wenyeji wa mchezo wa mkondo wa kwanza Aprili 17.

Simba SC wataanzania nyumbani kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Orlando Pirates

Simba wamewajua wapinzani wao baada ya kufanyika kwa droo ya kupanga michezo ya robo fainali na nusu fainali ya kombe la shirikisho iliyofanyika leo Aprili 05, 2022. Makao makuu ya CAF Cairo nchini Misri.

Kwa mujibu wa droo hiyo endapo kama wekundu wa msimbazi Simba SC wakifanikiwa kuvuka hatua ya robo fainali basi katika hatua ya nusu fainali watakutana na mshindi wa jumla wa mchezo wa robo fainali inayowakutanisha Al Ittihad dhidi ya Al Ahly Tripoli zote zikiwa ni timu kutoka Libya.

Kwa upande mwingine klabu ya Pyaramids ya Misri imepangwa kucheza dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo na Al Masry ya Misri wataminyana na RS Berkane ya Morocco. Michezo ya mkondo wa kwanza itachezwa Aprili 17 na ile ya mkondo wa pili ni Aprili 24, 2022.