Jumatatu , 11th Jul , 2016

Rais wa Simba, Evans Aveva amesema kuwa sasa ni rasmi wameshampa Kiiza mkono wa kwaheri na hakuna tena kilichopo baina yao na zaidi wamemtakia kila la kheri huko aendako pamoja na kumshukuru kwa mchango wake mkubwa katika timu hiyo.

Hamis Kiiza

Tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Bara 2015/2016, kumekuwa na taarifa mbalimbali juu ya kutemwa kwa mshambuliaji huyo kutokana na sababu za utovu wa nidhamu lakini hakukuwa na kiongozi aliyewahi kuthibitisha kuhusiana na hilo zaidi ya kutoa kauli zenye viashiria vya hali kama hiyo.

Aidha, ilielezwa kuwa Kiiza anaweza kutemwa pamoja na Mganda mwenzie, Juuko Murshid kutokana na kufuata mkumbo wa kugoma kuichezea timu hiyo mpaka wapewe mishahara yao.

Kiiza aliyewahi kuichezea klabu ya Yanga anaungana na wachezaji wengine wa kigeni waliotemwa msimu huu ambapo ni Mkenya, Raphael Kiongera, Mrundi, Emiry Nimubona na Mganda, Brian Majwega.