Ijumaa , 12th Jun , 2015

Simba SC imesema haitafanya kikao chochote na mchezaji wake, Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ kama ilivyoshauriwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika taarifa yake, Rais wa Simba SC, Evans Aveva amesema kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu kilichofanyika jana, pamoja na mambo mengine kilijadili suala la Singano.

Aveva amesema klabu itakuwa tayari kufanya naye mazungumzo muda muafaka utakapofika, kwa mujibu wa kanuni na taratibu za mikataba.

Juzi, TFF iliitaka Simba SC kuketi na Singano ‘Messi’ kujadili namna ya kuingia Mkataba mpya, baada ya pande zote kuafiki Mkataba wa sasa una hitilafu.

Katika kikao hicho kilichofanyika, makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam, Simba SC iliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati yake ya Utendaji, Collins Frisch wakati Messi aliandamana na Mussa Kisoky wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA).

TFF ilisema kaatika kikao hicho pande zote zilitambua utata ulio ndani ya mikataba iliyokuwepo ambayo kimsingi iliingiwa kabla ya uongozi wa sasa wa Simba SC.

TFF ikasema, pande hizo mbili zimekubaliana kuanza mazungumzo ya makubaliano mapya kwa ajili ya Mkataba utakaoanza msimu mpya wa 2015/2016.

Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo kwamba imeghushi Mkataba wake.

Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.

Lakini baada ya kikao pamoja na taarifa rasmi ya TFF, Messi alizungumza na vyombo vya Habari akisema yeye ni mchezaji huru ana hiari ya kuzungumza na Simba au klabu yoyote kwa ajili ya Mkataba mpya.

Na Kisoky wa SPUTANZA akasema wanalihamishia suala hilo kwenye Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji kutafuta haki zaidi.