Jumatano , 11th Feb , 2015

Klabu ya Simba imesema suala la mchezaji Shaaban Kisiga kutoonekana kambini kwa kipindi kirefu wanalipelekeka katika vikao husika ili kuweza kujadiliwa.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Stephen Ally amesema mchezaji huyo aliyeondoka kambini mara baada ya kumaliza mechi dhidi ya Mbeya City hakutoa taarifa na hawajapata maelezo yoyote kutoka kwake licha ya kumuandikia barua aelezee kilichomsibu.

Ally amesema kwa kuwa Kisiga haoneshi nia ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo hawataendelea kumtafuta kwani hivi sasa wapo katika maandalizi ya Michuano inayoendelea ya Soka Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ally amesema, kitendo cha Kisiga kuondoka kambini bila taarifa sio cha busara kwani kama ana tatizo sheria za kufuata anazijua na angeruhusiwa.

Kwa upande mwingine Ally amesema, Suala la Kocha msaidizi Suleiman Matola kuhitaji kuondoka kuacha kuifundisha klabu hiyo Uongozi utakaa na kuzungumzia suala lake lakini mpaka sasa Matola bado ni Kocha wa Klabu hiyo.