Ijumaa , 27th Feb , 2015

Ligi kuu soka Tanzania Bara inaendelea kesho kwa timu ya Simba kuwakaribisha wajelajela Tanzania Prisons mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Kocha wa Tanzania Prisons, David Mwamaja amesema wamejipanga vizuri kwa ajili ya pambano hilo ambalo anaamini watajitoa katika nafasi waliyonayo hivi sasa.

Mwamaja amesema, katika msimamo wanaonesha wapo chini na hiyo ni hali iliyojitokeza na sio kwamba timu ni mbaya na vijana wake wamejitolea kucheza kwa bidii ili kuweza kupata mafanikio mazuri.

Mwamaja amesema wanajua Simba watakuwa na hasira baada ya kutoa sare katika mchezo uliopita dhidi ya Stand United lakini anaamini jitihada za timu na ushirikiano zinafanikisha kufikia malengo.

Kwa upande wake nahodha wa Timu hiyo, Raulian Mpalile amesema, Simba ni timu nzuri na kwa vyovyote vile wanaamini mchezo utakuwa ni mgumu lakini kwa jinsi walivyojiandaa wanaamini watatoka na Pointi tatu katika mchezo huo.