Jumanne , 20th Sep , 2022

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kesho Septemba 21,2022 inawaaga mashujaa wa taifa, Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake (Serengeti Girls U17) kwa ajili ya kwenda nchini Uingereza kufanya maandalizi ya mwisho ya kushiriki mashindano ya dunia.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa anatarajiwa kuwaongoza watanzania wote kuwaaga mashujaa hao kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa tano asubuhi.

Aidha, katika hafla hiyo ya kuwaaga wachezaji hao, Waziri Mchengerwa atawakabidhi Bima za Afya na vifaa vya michezo kwa ajili ya mashindano hayo.

Mara kwa mara, Mhe. Mchengerwa amekuwa akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali kwa sasa ni kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya michezo ili michezo itumike kuitangaza Tanzania kimataifa na kuinua kipato cha wachezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Timu ya Serengeti Girls inaandika historia ya kuwa timu ya pili ya soka nchini kuingia kwenye mashindano ya dunia baada ya Timu ya soka ya walemavu ambayo ilifuzu kuingia kwenye mashindano ya dunia ya soka kwa wenye Ulemavu ambayo yanaanza mwanzoni mwa mwezi Oktoba nchini Uturuki.

Tayari timu hiyo ilishaondoka nchini kuelekea Uturuki kwa ajaili ya maandalizi ya mashindano hayo tangu Septemba 13 mwaka huu.

Mbali na timu hizo Timu ya Taifa ya Wanaume ya Kabbadi na timu ya wanawake tayari nazo zimefuzu kuingia kwenye mashindano ya dunia ya mchezo huo na kufanya jumla ya timu nne kuingia kwenye mashindano ya dunia katika kipindi kifupi cha Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu