
Katibu mkuu wa TFF Mwesigwa Celestine amesema ni jambo la kujisifia kwa Tanzania kwa wachezaji hao kwa kufanikiwa kucheza na kutwaa Ubingwa wa Afrika na kumuwezesha Samatta kuweza kuibuka mfungaji bora.
Mwesingwa amesema, mafanikio ya Samatta na Ulimwengu yanafungua milango ya mafanikio kwa vijana wengine wa Tanzania wanaoibuka katika soka.
Baada ya ushindi huo, klabu ya TP Mazembe itaiwakilisha Afrika katika michuano ya klabu bingwa ya dunia itakayochezwa Desemba 10 mpaka 20 Japan.
Ushindi huo umempa nafasi kubwa Samatta ya kuweza kuibuka na tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ambaye mpaka sasa ameingia kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania tuzo hiyo.
Mshindi wa tuzo hiyo ataamuliwa kwa kura zitakazopigwa na makocha pamoja na wakurugenzi wa ufundi wa nchi wanachama wa shikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF).
Pia shirikisho hilo limetoa orodha nyingine ya wachezaji wanaowania tuzo ya Afrika ambayo inahusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani au nje ya Afrika ambapo tuzo hiyo itakabihiwa kwa mshindi Alhamisi, 7 January 2016 Abuja, Nigeria.