Jumatatu , 11th Oct , 2021

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, Oscar Milambo amesema ni kweli nahodha wa Taifa Stars hakuwa kwenye kiwango chake kilichozoeleka na wao walifahamu hilo kwa muda mrefu wakiamini lingefikia kikomo.

Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Milambo akizungumza na Waandishi wa Habari.

Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya nyota huyo anayekipiga katia Klabu ya Royal Antwerp ya Ubelgiji kwa mkopo, kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa pili kufuzu fainali za kombe la Dunia dhidi ya Benin ambao Tanzania ulishinda ugenini kwa bao 1-0.

Milambo amesema Samatta hakuwa kwenye kiwango chake kilichozoelekea tangu aondoke Ubelgiji na kutimkia Uingereza ambapo hakuwa na mazingira mazuri ambayo yalimnyima furaha ya kuifanya kazi yake .

''Kwa siku za nyuma Nahodha Mbwana Samatta hakuwa akicheza kwenye uwezo wake wa kawaida uliozoeleka,sisi tulikuwa tunaelewa sababu ni zipi,hakuwa ametulia tangu atoke Ubelgiji na kutua Uingereza, hakukaa kwenye mazingira ambayo yangempa faraja ya kufanya kazi yake kwa furaha, lakini hivi karibuni amerejea katika ubora wake na tumeona anachokionyesha kwenye timu ya Taifa''Oscar Milambo Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF .

Wakati huohuo Milambo amesema wanafurahishwa na kiwango cha Simon Msuva ambacho kimekuwa cha muendelezo huku akipongeza jitihada za Dismus Novatus aliyeonyesha kiwango cha juu tangu ajumuishwe katika kikosi cha timu ya Taifa.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa ufundi amesema wanajipanga kumuwezesha Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ili apate muda mzuri wa kuiandaa timu kabla ya kucheza na Congo DR na Madagascar ili tufuzu fainali za kombe la Dunia.