Ijumaa , 17th Mei , 2019

Sasa hivi ni furaha kubwa kwa mashabiki wa klabu ya KRC Genk, baada ya usiku wa jana kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu nchini Ubelgiji maarufu kama 'Jupiter Pro League' msimu 2018/19.

Genk, mabingwa wa Ligi ya Ubelgiji 2018/19

Genk imeshinda ubingwa baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Anderlecht, ikifikisha jumla ya pointi 51 katika msimamo wa 'Playoffs' ambapo pointi hizo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika mchezo mmoja uliosalia kabla ya msimu kumalizika.

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta amechangia kwa kiasi kikubwa ubingwa huo kutokana na kiwango kikubwa alichokionesha mpaka sasa, akiwa amefunga mabao 23 ya ligi mpaka sasa akiwa anaongoza mbio za ufungaji bora wa ligi hiyo, dalili nzuri zipo kwake kutokana utofauti wa mabao baina yake na mchezaji anayefuatia, Hamdi Harbaoui wa Zulte-Waregem ambaye ana mabao 18.

Katika msimu huu, Samatta amecheza mechi 35, mara 2 kati ya hizo akitokea benchi mpaka sasa na kufunga jumla ya mabao hayo 23, akitoa assist 5.

Rekodi ya Genk ya Samatta na ubingwa 

 

Ubingwa huo ni wa nne katika historia ya klabu ya Genk, ambapo ubingwa wake wa kwanza ilishinda mwaka 1999 na kutokana na kushinda ubingwa, Genk imejikatia tiketi ya kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.