Jumanne , 29th Oct , 2024

Halmashauri ya jiji la Tanga imeongeza muda wa dirisha la maombi ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kupata idadi ya wakopaji inayolingana na kiasi cha shilingi bilioni 3 ambazo zimetengwa na serikali kwa ajili ya kuyawezesha makundi hayo kiuchumi.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Simon Mdende,

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mhandisi Juma Hamsini, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Simon Mdende, amesema kwamba muda ulioongezwa ni siku 14 pekee kutoka tarehe 27 mwezi Oktoba hadi Novemba 10 mwaka huu. 

Mdende amebainisha kuwa mpaka sasa vikundi zaidi ya 340 katika Halmashauri ya Jiji la Tanga vimepeleka maombi kwa ajili ya kusajili kwenye dirisha la mikopo hiyo ya asilimia 10 ambapo wanawake ni vikundi  211, vijana 119 na wenye ulemavu vikiwa 10.

"Tumeongeza dirisha kwa muda wa siku 14 pamoja na kuongeza dirisha hili lakini bado tumepata mafanikio sababu mpaka sasa jumla ya vikundi 340  vimeleta maombi kwa ajili ya hatua ya kwanza ya usajili na hatua ya pili ni kuomba mkopo, ukiangalia uwiano bado kuna nafasi kubwa hususani kwa vijana na watu wenye ulemavu kwajili ya bilioni 3 tulizotenga," amesisitiza Mdende.